Zitto Kabwe Kuliaga Bunge Rasmi

Thursday, March 19, 2015


MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema) jana aliteta faragha na Spika wa Bunge, Anne Makinda kushauriana naye kama ajiondoe kwenye ubunge baada ya chama chake kutangaza kumvua uanachama.
 
Lakini pia mbunge huyo jana hiyo jioni alipanga kuonana na spika wa zamani Samuel Sitta kuzungumza naye kuhusu suala hilo, ambalo habari za uhakika zinaeleza kuwa amedhamiria kuliaga Bunge hata kabla ya chama chake kuwasilisha barua ya kumvua uanachama kwa spika.
 
Akizungumza na mwandishi jana, Zitto ambaye hakukubali au kukanusha habari hizo, alisema kwamba atatangaza kujiondoa kwenye ubunge ama la, mara atakaposhauriana na spika Makinda pamoja na Sitta.
 
Zitto, ambaye jana habari zilitapakaa kuwa ataliaga Bunge, alimwambia  mwandishi kuwa habari hizo zinaweza kuwa na ukweli, lakini hatima yake itajulikana mara atakapokutana na viongozi hao ambao alisema katika kipindi chake cha ubunge cha miaka 10 walimlea bungeni.
 
Zitto alisema, “Kama hizo fununu zipo zitajulikana hivi karibuni, lakini kwanza ni lazima nishauriane na Makinda na Sitta, hawa wamenilea katika maisha yangu ya ubunge wakiwa viongozi wangu, hivyo siwezi kufanya jambo lolote linalogusa ubunge bila wao kushauriana nao.
 
“Hivi nakwenda kwa spika nyumbani kwake kwa sababu nina miadi naye na baadaye nitakwenda kuongea na Sitta…baada ya hapo nitakwambia kitakachofuata,” alisema Zitto.
 
Zitto ambaye alifika bungeni jana, alishiriki kikao cha kwa kuuliza swali la nyongeza na baadaye alishiriki kuchangia kwenye muswada wa sheria ya kuratibu ajira za wageni nchini.
 
“Jamani mimi bado ni mbunge si mmeniona nimeshiriki kikao cha leo, hayo mengine yatajulikana baadaye,” alisema Zitto.
 
Ubunge wa Zitto utakoma pale chama chake cha Chadema kitakapoandika barua kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo pia itamwandikia barua spika kumjulisha kuwa jimbo hilo liko wazi.

No comments:

Post a Comment