Maiti 13 wazikwa kaburi la pamoja.. INGIA HAPA

Wednesday, April 15, 2015

Waombolezaji wakizika miili ya watu 13 walioteketea kwa moto katika ajali ya Basi la Nganga na Fuso iliyotokea Iyovi, Ruaha Mbuyuni. Mazishi hayo yalifanyika jana katika Kijiji Nyavisi Ruaha, wilayani Kilosa, Morogoro. Picha ndogo ndugu wa mmoja wa marehemu wakilia wakati wa mazishi hayo. Picha na Juma Mtanda     
Morogoro. Maiti 13 kati ya 19 za watu waliopoteza maisha katika ajali ya Basi la Nganga Express na lori iliyotokea juzi eneo la Iyovi, Milima ya Udzungwa mkoani Morogoro wamezikwa jana katika kaburi la pamoja eneo la Msamvu mkoani hapa.

Simanzi na vilio vilitawala katika eneo hilo wakati miili ya watu hao ilipofikishwa hapo saa saba mchana kabla ya mazishi hayo kuanza ya saa 8.30 mchana.
Viongozi wa dini zote walifanya misa za kuwaombea marehemu hao waliopoteza maisha katika ajali hiyo ambayo baada ya kutokea, basi na lori hilo aina ya Fuso yaliteketea kwa moto na abiria waliokuwamo.
Akizungumza katika mazishi hayo, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, John Henjewele alisema tukio hilo ni la kusikitisha na la tofauti ambalo limeitia simanzi nchi nzima. “Ni tukio la nadra sana, lakini pia naweza kusema ni la kizembe kwa sababu tayari tumejua chanzo cha ajali hiyo,” alisema. Henjewele alisema wamepata malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu madereva wanaoendesha magari ovyo.
“Nawapongeza vijana wa eneo hili kwa kusaidia kutoa miili kwenye magari licha ya kuwa moto ulikuwa unawaka,” alisema Henjewele katika mazishi hayo yaliyohudhuriwa pia na Kiongozi wa ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe.
Miili ya abiria wengine sita, imetambuliwa na ndugu zao ilikohifadhiwa katika Hospitali ya Mtakatifu Kizito, Mikumi Wilaya ya Kilosa. Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo aliwataja marehemu waliotambuliwa katika ajali hiyo kuwa ni Hadija Legembo (35), mkazi wa Kilombero; Lidya Ndongwe (16), mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Mtakatifu Francis Mbeya na Ester Mgimba (30), mkazi wa Njombe. Wengine ni Nelson Patrick, mtoto wa miaka miwili mkazi wa Njombe; Marietha Ponsiano (19) mkazi wa Kilombero; Mengo Njagaje (30), mkazi wa Mbeya. Kamanda Paulo aliwataja majeruhi 10 wa ajali hiyo kuwa ni Majaliwa Elisha (21), mwanafunzi wa kidato cha tatu shule ya St Mary Mbeya; Linda Jonathan (26), mkazi wa Mbeya, Rose Seth (18), mwanafunzi wa kidato cha nne Shule ya Sekondari Sanje Kilombero na Elias Augustino (36), mkazi wa Kilombero. Majeruhi wengine ni Batista Emmanuel (44), mkazi wa Mbeya, Abubakar Athumani (36), mkazi wa Ruaha, Emmanuel Omarino (18), mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Konsolata Iringa; Teresia Kusila (25), mkazi wa Ruaha, Shafii Mussa (25), mkazi wa Kilombero na Anyindwile Elia (30), kondakta wa Basi la Nganga Express.
Chanzo cha ajali
Kamanda Paulo alisema basi hilo lilipata ajali likiwa linatokea Kilombero kwenda Mbeya likiwa na abiria 27.
Alisema lilikuwa likiendeshwa na Batista Emanuel (44) na lilipofika Iyovi, kilomita 75, kutoka Mji wa Mikumi, dereva huyo alihama na kwenda upande wa kulia zaidi mwa barabara na kugongana uso kwa uso na Fuso ambalo dereva wake bado hajafahamika.

MWANANCHI

No comments:

Post a Comment